RAIS MWINYI NA AFRICA SUMMIT 2025

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itaendelea kuwa daraja muhimu la kuiunganisha Afrika na Ulimwengu katika masuala ya Ubunifu, Tafiti na Uimarishaji Endelevu wa Elimu ya juu kwa ajili ya Maendeleo.    

Rais Dkt,  Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Mkutano wa Elimu ya juu na Teknolojia Afrika uliofanyika Hoteli ya Golden Tulip ,Uwanja wa Ndege.       

Amefahamisha kuwa suala muhimu ni kuwa na Ushirikiano na Vyuo vikuu na Taasisi za Elimu ya juu Afrika na Ulimwenguni ili kutoa fursa ya Kuungana na Vyuo kwa ajili ya Ufanyaji waTafiti, Ubunifu na Teknolojia ili kuimarisha Elimu ya juu.    

Amesisitiza kuwa Zanzibar inaweza kuwa kituo muhimu kwa ajili ya kuendesha programu mbalimbali za Elimu ya juu kutokana na mazingira na kuwepo kwa Amani ya kudumu na utayari wa Serikali katika kuimarisha Taasisi za Kielimu katika kufanya Tafiti, Ubunifu na kubadilishana Uzoefu wa kitaaluma baina ya Mataifa.  

Akizungumzia Suala la teknolojia ya Akili Mnemba [Ai] Rais Dkt, Mwinyi amefahamisha kuwa Zanzibar haipaswi kubaki nyuma Katika matumizi ya Teknolojia pamoja na Akili mnemba lakini ni lazima ihakikishe inapata manufaa na Faida zake na kuhakikisha Udhibiti wa Athari za Akili mnemba ‘AI’ kwa Kushirikiana na Taasisi za kielimu za kimataifa.  

Aidha Rais Dkt,  Mwinyi amesisitiza kuwa Zanzibar imeiweka Sekta ya Elimu na Elimu ya Juu kuwa Sekta ya Kipaumbele katika kuleta Maendeleo,Fursa mbalimbali za Kiuchumi na Ushirikiano wa Taasisi.   

Ameeleza kuwa Kufanyika kwa Mkutano huo hapa Nchini ni hatua muhimu ya Ushirikano wa Nchi za Afrika na kuwa sauti ya pamoja kuelekea Maendeleo Endelevu ya Elimu ya juu ,Ubunifu na Teknolojia.

*Naye* Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohammed Mussa amesema Zanzibar inaendelea na Mabadiliko makubwa ya Mitaala ya kielimu ili kuendana na mahitaji ya mabadiliko ya Teknolojia ili kuzalisha Wahitimu wenye sifa na Uwezo kielimu. 

Ameeleza kuwa Maendeleo ya Elimu ya juu,Ubunifu , Tafiti na Teknolojia sio suala la Serikali pekee bali linahitaji Ushirikiano baina ya Taasisi za kielimu za ndani ya Nchi na za kimataifa.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000